UWASILISHAJI WA MUONGOZO WA MAWASILIANO NA SANDUKU LA MALALAMIKO KWA WANAFUNZI NA MAHABUSU ZANZIBAR.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC - Zanzibar) umeendelea kushirikiana na Chuo cha Mafunzo Zanzibar (ZIEO) na taasisi nyingine za haki za binadamu katika kuimarisha haki za binadamu Zanzibar.
Leo hii, ZIEO kupitia Naibu Kamishna DCP. Haji Hamdu Omar, imeongoza zoezi la utoaji wa muongozo wa uwasilishaji
malalamiko na mawasiliano kwa wanafunzi na mahabusu Zanzibar, pamoja na utoaji wa masanduku ya malalamiko katika vyuo vya mafunzo. Zoezi hili ni la Unguja na Pemba, kwa lengo kuu la upatikanaji wa haki endapo zitavunjwa katika mazingira ya vizuizi. Muongozo huo umeainisha masuala mbalimbali ikiwemo taratibu za kuripoti malalamiko, wajibu wa taasisi mbalimbali za haki, na hata makatazo kadhaa.
DCP. Haji Hamdu Omar ameipongeza timu nzima. Ameipendekeza na kusisitiza THRDC juu ya mafunzo ya utumiaji wa muongozo huu kwa maafisa wa jeshi la polisi, na mafunzo kwa watendaji wa magerezani. Mratibu wa THRDC Zanzibar, Bw. Baitani Mujuni amepokea na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo hayo.
Ikumbukwe ya kwamba, mchakato huu umefanywa na timu ya wadau wa haki za binadamu ambao ni ZIEO, THRDC, Mahakama kuu, Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Zanzibar Child Right Forum (ZCRF), na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP Office).
Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu - Zanzibar.