THRDC-ZANZIBAR YAONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA UTEKELEZAJI, UFUATILIAJI NA TATHMINI YA MUONGOZO WA MALALAMIKO WA WANAFUNZI CHUO CHA MAFUNZO

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) tawi la Zanzibar umeongoza kikao cha kwanza cha kamati ya ufuatiliaji na utaratibu wa Mwongozo wa kutoa malalamiko na
kuweka mikakati ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa
mwongozo wa malalamiko na mawasiliano kwa wanafunzi (watuhumiwa na wafungwa) magerezani Zanzibar leo tarehe 18 Julai 2023.
Kamati hiyo imeundwa na Mwongozo huu kwa lengo la kusimamia na kufuatilia utekelezaji na ufanisi wa Mwongozo huu
mpya ulioratibiwa na Chuo cha Mafunzo kwa ushirikiano na THRDC na wadau wengine. Washiriki hawa ni pamoja na mwakilishi kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Afisi ya Mwendesha
Mashitaka wa Serikali, Mahakama Kuu, Tume ya Haki za Binadamu (CHRAGG), Makao Makuu ya Polisi, Chama cha
Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Watoto Zanzibar (ZCRF), Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), na THRDC-Zanzibar.
Malengo ya mwongozo huu ni kutoa nafasi ya wanafunzi kuwasilisha malalamiko yao kwa njia zinazoratibiwa vizuri na kwa pamoja. Kamati imepanga mikakati imara ya usimamizi na ufuatiliaji wa uwasilishaji malalamiko ya wanafunzi walioko vizuizini pamoja na mikakati ya ndani ya kila Mdau wa haki katika kufanyia kazi malalamiko hayo yatakapofikishwa kwa taasisi zao.
Tayari masanduku ya Maoni kwa ajili ya utekelezaji huu yameshakabidhiwa kwa uongozi wa magereza kwa uwezeshaji
wa THRDC. Masanduku haya yatawekwa katika kila Bweni na maeneo yote ambayo wanafunzi wanaweza toa maoni yao kwa uhuru na kwa haraka zaidi. Kamati hii itakuwa inakutana kila baada ya miezi mitatu kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mwongozo huu.
THRDC pamoja na wadau wengine wamedhamiria kuifanya huduma ya magereza Visiwani Zanzibar iwe ya kuigwa na ya mfano hapa barani Afrika. Mikakati mingine ya maboresho ya kisera na kisheria inaendelea kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kujirekebisha kitabia na kurudi kwenye jamii kama watu wema na wenye kuweza kuendelea na maisha.

Imetolewa na THRDC - Zanzibar.