WARAKA WA ASASI ZA KIRAIA 13 ZA AFRIKA KWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ZIKIMSIHI AWAACHILIE HURU WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU, WAANDISHI WA HABARI NA WAFUNGWA WA KISIASA NCHINI TANZANIA

Nairobi, Kenya

Jana tarehe 4 Mei 2021, majira ya mchana wakati Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwasili nchini Kenya katika ziara yake fupi ya siku mbili (2) nchini humo, Asasi za Kiraia (AZAKi) 13 za Afrika kutoka nchini Kenya, Tanzania, Uganda na Ethiopia zikiongozwa na shirika la Defenders Coalition-Kenya zilimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kwa salamu za pongezi kwa kuwa Rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia waraka wao wa pamoja.

Pia waraka huo ulimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake katika maadhimisho ya Miaka 57 ya Muungano wa Tanzania; wa kutoa msamaha kwa wafungwa 5,001 waliokiwa wakikabiliwa na adhabu mbalimbali za vifungo katika magereza nchini Tanzania.

Waraka huo zaidi ulilenga kumsihi Rais Samia Suluhu Hassan kwanza kama mama na mlezi wa taifa, mwanaAZAKi wa muda mrefu na kama Mkuu wa Nchi awaachilie huru pia watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari pamoja na wafungwa wa kisiasa ambao bado wanasalia magerezani. Na pia kukemea waziwazi ukiukwaji wa haki za watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wanaharakati wa kisiasa nchini.

Idadi ya wafungwa iliyotajwa na mashirika hayo kupitia waraka wao ni takriban wafungwa 100.

Kusoma zaidi tembelea ukurasa huu: The final press release

https://defenderscoalition.org/appeal-to-tanzanias-president-her-excellency-samia-suluhu-hassan-to-release-all-human-rights-defenders-journalists-and-political-activists-in-tanzania/