TUZO YA HAKI ZA BINADAMU KWA RAIS SAMIA, THRDC

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), hii leo Mei 13,2022 umemtunuku  tuzo maalum Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia mchango wake katika kuchagiza uimarishwaji wa haki za binadamu nchini.

Rais Samia amepewa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya THRDC, Jaji Mstaafu, Joaquine De mello, katika sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya THRDC yanayofanyika jijini Dar es salaam.

“Tumekupa tuzo hii Rais Samia kwa kuthamini na kutambua kazi kubwa unayofanya unayofanya kwa kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu wanafanya kazi na shughuli zao kwa uhakika na wakati pasipo bughuza yoyote,” amesema Jaji Demello.

Kwa upande wake Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema watetezi wa haki za binadamu wameandaa Makala maalumu kuhusu mchango wa Rais Samia katika uimarishaji haki za binadamu.

“Kazi yako katika eneo la haki za binadamu ni kubwa sana na inaonekana kote Tanzania na duniani, taarifa rasmi kuhusu mchango wako katika kulinda na kueneza haki za binadamu kwa kipindi cha mwaka mmoja imeandaliwa kwa lengo la kutambua na kuweka kumbukumbu kwa mambo uliyofanya,” amesema Olengurumwa.

Makalla hiyo ya video yenye muda wa takribani dakika tano, imeoneshwa kwenye maadhimisho hayo mbele ya Rais Samia ikielezea masuala mbalimbali ya haki za yaloyotekelezwa na Rais Samia katika kipindi cha mwaka mmoja aliopo madarakani ikiwemo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kufunguliwa kwa akaunti za THRDC zilizokuwa zimefungiwa.

Watetezi TV
Dar es salaam
13/05/2022