Mnamo tarehe 25 na 26 Mei 2024, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ulitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watetezi wa haki za jamii za kifugaji na watu wa asili nchini. Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika mkoani Arusha yakijumuisha watetezi wa haki za jamii ya wafugaji 55 kutoka taasisi mbalimbali nchini Tanzania.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa, alieleza lengo la mafunzo hayo kuwa ni kuwajengea uwezo watetezi wa haki za jamii za kifugaji na watu wa asili nchini kuhusiana na haki zao, wajibu wao na kuwawezesha kutambua mazingira hatarishi na namna ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi wao. Pia alieleza kuwa anatambua mchango mkubwa wa watetezi wa haki za binadamu katika jamii hiyo hasa vijana na wanawake amabao wamekuwa kipaumbele katika kuitetea jamii hiyo. Mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuwajengea uwezo wa kutambua haki na wajibu wao pamoja na Sheria zinazowasimamia ili waweze kufanya kazi zao za utetezi kwa ufanisi zaidi.
Katika mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utetezi THRDC Wakili Paul Kisabo alielezea Mikataba, Sheria na Sera zinazowatambua na kuwalinda watetezi wa haki za jamii ya kifugaji na watu wa asili nchini. Mbali na sheria, Wakili Kisabo aliwafundisha pia washiriki wa mafunzo hayo kuhusu wajibu wao ikiwa ni pamoja na kulinda na kustawisha haki za wafugaji na haki za binadamu kwa ujumla.
Vilevile, Wakili Olengurumwa aliwafundisha washiriki kuhusu namna ya kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi za utetezi katika jamii zao, hii ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kutambua matishio ya kiusalama na namna ya kutengeneza mpango bora wa kiusalama ili kuboresha mazingira yao na kuhakikisha wanatetea haki za wafugaji katika mazingira salama.
Aidha, Mhe. Alais Morindati ambaye ni mtetezi wa haki za wafugaji wa muda mrefu aliwafundisha washiriki wa mafunzo kuhusu historia ya watetezi wa jamii za kifugaji, kufahamu asili yao, na namna bora ya kushirikiana na wadau wengine ili kuboresha haki za jamii za kifugaji nchini.
Zaidi, washiriki waliweza kujadili kwa pamoja changamoto wanazokutana nazo na kuweza kutengeneza mpango mkakati wa namna ya kukabiliana na changamoto hizo katika utetezi wa haki za wafuganji nchini.
Mwisho, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mhe. Mrinda Mshota wakati anafunga mafunzo hayo, alishukuru na kuipongeza THRDC kwa mafunzo hayo muhimu. Mhe. Mshota alieleza jitihada ambazo CCWT imekuwa ikifanya katika kuboresha haki za wafugaji ikiwemo kufanya uchaguzi wa viongozi zaidi ya wilaya 90 na kuanizisha wakala wa usimamizi wa mifugo nchini. Vilevile alieleza changamoto wanazopitia watetezi wa haki za jamii ya wafugaji ikiwemo kutaifishwa kwa mifugo au kutozwa faini kubwa kwa wafugaji na wafugaji kuondolewa katika ardhi yao ya miaka yote. Hivyo, aliahidi kukiimarisha chama cha wafugaji na kushirikiana na serikali kwa ukaribu zaidi ili kutoa suluhu ya changamoto wanazopitia wafugaji wote nchini.
Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Dar es Salaam, Tanzania
Juni 28, 2024